[ad_1]
Na IRENE MUGO
HALMASHAURI ya Kusimamia Majanichai Kenya imetangaza kwamba bei ya mazao hayo imepungua kwa asilimia 12 duniani kutokana na uzalishaji kwa wingi kutoka kwa mataifa mbalimbali na ukosefu wa soko.
Kwa muda wa miezi tisa iliyopita kuanzia Machi 2020, mwaka wa kifedha uliopita, bei ya majanichai imepungua kutoka kwa Sh271 hadi Sh239 kwa kila kilo.
Kwa muda huo, uzalishaji ulipungua kwa asilimia 8.6 baada ya wakulima kuvuna kilo 218.9 ikilinganishwa na kilo 239.6 zilizotayarishwa kiwandani muda huo, mwaka uliopita.
Licha ya kushuka kwa bei hiyo, bei ya KTDA imepanda kwa asilimia 17 ikilinganishwa na bei ya wastani ya kunadi majanichai jijini Mombasa ambayo ni Sh204.
Halmashauri hiyo ilieleza kwamba sawa na mazao mengine, bei ya majanichai imekuwa ikipungua kwa muda wa miaka mitatu duniani kutokana na wingi wa mazao na uchumi usiodhabiti wa mataifa yaliyokuwa yakinunua mazao hayo sana zamani.
“Kuna majanichai tele katika masoko ya nje na hili linafanya bei iwe chini. Japo tumepungua katika uzalishaji, hakuna ukosefu wa mazao hayo katika mataifa ambayo huwa ni soko kubwa kwa Kenya na nchi nyinginezo,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa KTDA, Bw Alfred Njagi.
“Hata bei ya mnada ya kuuza majanichai imepungua si hapa Kenya pekee, bali ulimwenguni kote,” akaongeza.Mamlaka ya Kilimo na Vyakula (AFA) pia imetaja athari ya virusi vya corona kama sababu kuu ya kuendelea kupungua kwa bei ya majanichai.
“Mataifa yaliyokuwa soko la Kenya, yamepunguza uagizaji wa majanichai kutokana na ukosefu wa uwezo wa kuyanunua kama zamani. Uchumi wa mataifa mengi umeathirika kutokana na kuchipuka kwa virusi vya corona na kushuka kwa thamani ya bei ya dola na sarafu nyingine za kimataifa,” ikasema taarifa ya AFA kuhusu mauzo ya majanichai mnamo Februari.
AFA pia inasema hazina kubwa ya majanichai na uzalishaji kwa wingi katika baadhi ya nchi pia umechangia kupungua kwa bei ila hali huenda ikabadilika mwaka huu kutokana na hali ya kuridhisha ya hali ya hewa.
“Mwaka huu utakuwa tofauti na mwaka jana kwa sababu ya utabiri wa wanasayansi kuwa hali ya hewa itakuwa shwari. Hata hivyo, uzalishaji hautapanda sana na kiwango cha chini kilichoshuhudiwa mwanzo wa mwaka huu huenda kikaendelea hadi mwisho wa mwaka,” ikaongeza AFA.
Hapa Kenya, uzalishaji wa juu wa majanichai unahusishwa na hali ya kuvutia ya hali ya hewa pamoja na ekari nyingi za ardhi ambako kilimo hicho huendelezwa.
Mwaka jana, wakulima wadogo wadogo wa majanichai chini ya KTDA walichangia uzalishaji wa kilo 1.454 bilioni, Hii ilikuwa nyongeza ya asilimia 22 kwa kuwa kilo 1.13 bilioni zilizalishwa mnamo 2019.
Mataifa mengine ambayo yanakuza majanichai kwa wingi kama Rwanda, Sri Lanka na India pia yalizalisha kwa wingi katika muda huo ila bei ilisalia chini.
[ad_2]
Source link