Home » Burnley watoka nyuma na kunyima Aston Villa fursa ya kuingia 8-bora EPL – Taifa Leo
News

Burnley watoka nyuma na kunyima Aston Villa fursa ya kuingia 8-bora EPL – Taifa Leo

[ad_1]

Na MASHIRIKA

KIUNGO Chris Wood alifunga bao la dakika za mwisho na kusaidia Burnley kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha Aston Villa kwa magoli 3-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumatano usiku uwanjani Turf Moor.

Villa walikuwa wakijivunia uongozi wa mabao 2-1 kufikia dakika ya 76 kabla ya Dwight McNeil kusawazisha mambo kisha Wood kufunga bao la ushindi kwa upande wa Burnley.

Villa walitamalaki mchezo katika kipindi cha kwanza na wakawekwa uongozini kupitia kwa Ollie Watkins aliyekamilisha krosi ya Matt Targett katika dakika ya 14.

Baada ya kipa Nick Pope kupangua makombora aliyoelekezewa na Villa, Burnley walisawazisha mambo kupitia Ben Mee kabla ya wageni wao kurejea uongozini kunako dakika ya 68 kupitia kwa kiungo Jack Grealish.

Burnley walishuka dimbani kwa minajili ya mchuano huo wakijivunia kufunga mabao matano pekee kutokana na mechi nane zilizopita za EPL ugani Turf Moor. Hata hivyo, ushindi uliwapunguzia presha ya kuteremshwa ngazi ligini kwenye kampeni za muhula huu.

Burnley kwa sasa wanashikilia nafasi ya 15 kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 22, tisa mbele ya Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion na Sheffield United wapo katika hatari ya kushushwa ngazi mwishoni mwa muhula huu.

Kwa upande wao, Villa wameshinda mchuano mmoja pekee kati ya sita iliyopita katika mashindano yote na kocha Dean Smith alisema kwamba vijana wake watajutia kupoteza nafasi nyingi za wazi ambazo vinginevyo zingewavunia ushindi.

Villa kwa sasa wanafunga mduara wa 10-bora kwa alama 29 sawa na Southampton.

Burnley kwa sasa wanajiandaa kupepetana na Chelsea ya kocha Thomas Tuchel uwanjani Stamford Bridge mnamo Januari 31 kabla ya kuwaalika Manchester City siku tatu baadaye ugani Turf Moor.

Kwa upande wao, Villa watawaendea Southampton ugani St Mary’s mnamo Januari 30 kabla ya kushuka dimbani kukwaruzana na West Ham United mnamo Februari 3, 2021.

[ad_2]

Source link