[ad_1]
Na KNA
MBUNGE wa Garissa Mjini Aden Duale ametoa wito kwa vyama vya kisiasa nchini kuungana kuokoa Mswada wa Mageuzi ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) kwa kupitisha baadhi ya mapendekezo yake kupitia bunge.
Akiongea kwenye hafla ya kuchanga fedha mjini Garissa, Jumamosi, Duale ambaye ni kiongozi wa zamani wa wengi bungeni, alisema mahakama imeonekana kuwa kizingiti kikuu dhidi ya kufanyika kwa kura ya maamuzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
“Itachukua muda mrefu kwa kesi ya rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyoharamisha BBI kusikilizwa na kuamuliwa. Kisha huenda rufaa nyingine dhidi ya uamuzi wa mahakama hiyo ikawasilishwa katika Mahakama ya Juu. Kwa hivyo, mahala bora pa kushughulikia mswada huu ni bungeni,” akasema.
Bw Duale alisema japo alipiga kura ya kupinga Mswada wa BBI bungeni Aprili, yuko tayari kuunga mkono mradi kaunti za Kaskazini mwa Kenya hazitapoteza maeneo bungeni.
“Hatuna shida na BBI ikiwa hatutapoteza maeneobunge ya Ijara na Wajir Kusini. Ningetaka kuuliza vyama vikuu vya kisiasa kuungana kwa sababu Katiba inaruhusu katiba kufanyiwa mageuzi kupitia bunge. Wabunge wapewe nafasi ya kupitisha vipengele vya mswada wa BBI ambavyo havihitaji kuidhinishwa katika kura ya maamuzi huku tukisubiri mwelekeo kutoka mahakama zetu,” mbunge huyo wa Garissa Mjini akasema.
Bw Duale, ambaye ni mwandani wa Naibu Rais William Ruto, ni mmoja wa wabunge 83 waliopiga kura ya LA kupinga mswada wa BBI bungeni mapema mwezi huu wa Mei.
Mswada huo ulipitishwa baada ya kuungwa mkono na wabunge 235 baada ya kujadiliwa kwa siku kadhaa.
Wazo la katiba kufanyiwa marekebisho kupitia bunge sasa limepata uungwaji mkono kutoka kwa Spika wa Bunge Justin Muturi na wabunge kadhaa kutoka mirengo ya Tangatanga na Handisheki.
Wanasiasa wanaopendelea mfumo huo wanasema mfumo huo ni bora kwani hautagawanya Wakenya katika kura ya maamuzi itakayoibua joto la kisiasa nchini.
Mchakato wa kesi za kuhusu Mswada wa BBI unakisiwa kuwa utachelewesha maandalizi ya kura ya maamuzi ikizingatiwa kuwa uchaguzi mkuu wa 2022 unakaribia.
“Mswada huo wa marekebisho ya Katiba unahitaji kushughulikiwa bungeni kwa siku 90 ambapo umma utahitaji kushirikishwa. Nitawaunga mkono wale ambao wanataka kupitia mkondo huo, lakini sharti mswada huo uungwe mkono na thuluthi mbili ya wabunge,” Bw Muturi akasema Jumapili baada ya kuhudhuria Ibada ya Jumapili katika Kanisa moja la Anglikana mjini Embu.
Kundi la maseneta na wabunge kutoka mirengo mbalimbali ya kisiasa sasa wanataka bunge litwae kibarua cha kuifanyia mageuzi katiba, haswa vile vipengele ambavyo havihitaji kuidhinishwa kupitia kura ya maamuzi.
Vipengele hivyo ni kama vile kubuni kwa nyadhifa za Waziri Mkuu na Manaibu wake wawili, kuundwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani Bungeni na kuundwa kwa afisi ya kufuatilia utendakazi wa majaji almaarufu Ombudsman.
Mswada wa BBI ulipata pigo majuma mawili yaliyopita baada ya jopo la majaji watano kuamua kwamba mchakato huo ulikiuka katiba na hivyo ni haramu.
Tafsiri: CHARLES WASONGA
[ad_2]
Source link