Home » Kibarua cha kwanza cha kocha Tuchel kambini mwa Chelsea chakamilika kwa sare tasa dhidi ya Wolves ligini – Taifa Leo
News

Kibarua cha kwanza cha kocha Tuchel kambini mwa Chelsea chakamilika kwa sare tasa dhidi ya Wolves ligini – Taifa Leo

[ad_1]

Na MASHIRIKA

KOCHA Thomas Tuchel alianza kazi kambini mwa Chelsea kwa kuwaongoza waajiri wake kusajili sare tasa dhidi ya Wolves katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha uwanjani Stamford Bridge mnamo Januari 27.

Tuchel aliyeajiriwa Jumanne kuchukua nafasi ya Frank Lampard aliyetimuliwa Januari 25, alisimamia mchuano wake wa kwanza kambini mwa Chelsea baada ya kuwaongoza kwenye kipindi kimoja pekee cha mazoezi mnamo Januari 26.

Matokeo ya Chelsea yalipania kumkumbusha Tuchel kuhusu uzito na ugumu wa kibarua kinachomkabili uwanjani Stamford Bridge.

Wolves walijibwaga ugani kwa minajili ya mchuano huo wakilenga kusajili ushindi wa kwanza ligini tangu Disemba 15, 2020.

Kipa Rui Patricio wa Wolves alifanya kazi ya ziada na kupangua makombora mazito aliyoelekezewa na Antonio Rudiger, Callum Hudson-Odoi, Mateo Kovacic na Ben Chilwell.

Chelsea walitamalaki mchuano huo, kumiliki asilimia kubwa ya mpira na kukamilisha jumla ya pasi 433 katika kipindi cha kwanza. Idadi hiyo ya pasi ndiyo ya juu zaidi kuwahi kukamilishwa na kikosi kinachodhibitiwa na Tuchel tangu Mei 2016.

Fowadi Pedro Neto wa Wolves alishuhudia kombora lake likibusu mwamba wa lango la Chelsea huku Willian Jose akimtatiza pakubwa kipa Edouard Mendy.

Katika mchuano wake wa kwanza kambini mwa Chelsea akiwa kocha, Lampard alishuhudia masogora wake wakilazimishiwa sare ya 1-1 kutoka kwa Leicester City uwanjani Stamford Bridge mnamo Agosti 2019.

Mechi dhidi ya Wolves ilishuhudia kocha Tuchel akiwaweka benchi wachezaji Mason Mount, Reece James na Tammy Abraham ambao walikuwa na uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza chini ya Lampard ambaye aliwawajibisha katika jumla ya michuano 39 ya awali.

Mwishoni mwa mechi hiyo, kubwa zaidi ambalo Tuchel aliwaahidi mashabiki wa Chelsea ni kutarajia makuu kutoka kwake na kumpa subira zaidi kabla ya matokeo bora kuanza kushuhudiwa.

Kocha huyo wa zamani wa Borussia Dortmund na Paris St-Germain (PSG) aliwataka pia wachezaji wake, hasa Kai Havertz na Timo Werner, kuzidisha kasi ya pasi zao na ziwe za hakika zaidi.

Chini ya Lampard, Chelsea walifungwa jumla ya mabao 77 kutokana na mechi 57 za EPL.

Wolves wanaonolewa na kocha Nuno Espirito Santo kwa sasa hawajashinda mchuano wowote wa EPL kati ya saba iliyopita na walijitosa uwanjani wakipigiwa upatu wa kuendeleza ubabe uliowashuhudia wakizamisha chombo cha Chelsea katika mchuano wa mkondo wa kwanza mnamo Disemba 15 ugani Molineux.

Wolves walitua jijini London wakijivunia kutia kibindoni alama mbili pekee kutokana na 18 walizokuwa na uwezo wa kujizolea baada ya mechi sita za awali. Mechi dhidi ya Chelsea ilikuwa ya kwanza kwa Wolves kutofungwa bao ligini tangu Oktoba 30, 2020.

Chelsea kwa sasa wanajiandaa kualika Burnley ugani Stamford Bridge mnamo Januari 31 huku Wolves wakitarajiwa kurejea jijini London kupepetana na Crystal Palace uwanjani Selhurst Park mwishoni mwa wiki hii.

[ad_2]

Source link