[ad_1]
Na GEOFFREY ANENE
BINGWA wa zamani wa dunia wa mbio za kilomita 21, Tegla Loroupe ameibua mjadala mkali kuhusu viatu vya kisasa vinavyotumiwa na nyota Eliud Kipchoge na wakimbiaji wengine kuvunja rekodi za dunia akisema wanaovitumia “wanadanganya”.
Loroupe, ambaye ni mwanamke wa kwanza Mwafrika kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 42, alisema katika mahojiano na Shirika la Habari la BBC kuwa viatu hivyo vinawapa wanaovitumia manufaa yasiyo ya haki.
Viatu ambavyo vimeundwa na kampuni ya Nike vilichangia pakubwa katika Kipchoge na Brigid Kosgei kuandikisha kasi ya juu kwenye marathon mwaka 2019.
Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kilomita 42 ya wanaume Kipchoge alitimka umbali huo kwa saa 1:59:40 katika mbio maalum za INEOS1:59 mjini Vienna nchini Austria mnamo Oktoba 12, 2019.
Naye mwanadada Kosgei alishinda taji la Chicago Marathon mnamo Oktoba 13, 2019 kwa rekodi ya dunia ya saa 2:14:04 nchini Amerika. Wakenya hao wawili walivalia viatu vya Nike Vaporfly wakipata mafanikio hayo na kuvifanya viendelee kukosolewa sana.
Ingawa Shirikisho la Riadha Duniani lilipiga marufuku viatu vilivyovaliwa na Kipchoge, Nike ilizindua sampuli nyingine ya viatu vya Alphafly visivyokiuka sheria mpya za shirikisho hilo kuhusu viatu vya mashindano.
“Mimi si shabiki wa viatu hivyo kwa sababu mkimbiaji hatumii nguvu zake za kibinadamu,” alidai Loroupe aliyejivunia kuvunja rekodi ya dunia ya kilomita 42 mara mbili. Loroupe alitimka umbali huo kwa saa 2:20:47 kwenye mbio za Rotterdam mwaka 1998 akifuta rekodi ya raia wa Norway Ingrid Kristiansen ya 2:21:06 iliyokuwa imedumu miaka 13. Aliimarisha rekodi yake mwenyewe aliposhinda Berlin Marathon 1999 kwa saa 2:20:43.
“Unadanganya, wewe si shujaa kwa sababu hutumii nguvu zako mwenyewe. Unaweza kuwa na kiatu kinachokufanya ukimbie kasi ya juu, lakini itakuwaje kama wale unaowashinda hawawezi kumudu bei viatu ya kama vyako? Inakaribiana na kutumia dawa za kusisimua misuli. Kivyangu, sioni tofauti kati ya kutumia dawa za kusisimua misuli na kutumia kiatu kinachokufanya ukimbie haraka.”
Muethiopia Kenenisa Bekele alivalia viatu vya utata vya Vaporfly akishinda Berlin Marathon mwaka 2019 kwa saa 2:01:41, sekunde mbili nje ya rekodi ya dunia ambayo Kipchoge aliweka katika mji huo wa Ujerumani mwaka 2018.
Mkenya Ruth Chepng’etich alitumia viatu vya kisasa vilivyotengezwa na teknolojia hiyo akiweka rekodi mpya ya kilomita 21 ya mbio za mseto ya saa 1:04:02 kwenye mbio za N Kolay Istanbul Half Marathon nchini Uturuki karibu wiki nne zilizopita (Aprili 4). Alinyoa sekunde 29 kutoka rekodi ambayo Muethiopia Ababel Yeshaneh (1:04:31) alitimka mjini Ras al-Khaimah mwezi Februari 2020.
Loroupe, 47, ambaye alishinda marathon 11 enzi yake zikiwemo London, New York na Berlin, anahisi kuwa viatu hivyo vinafaa kupigwa marufuku.
[ad_2]
Source link