[ad_1]
Na SAMMY WAWERU
JAJI Mkuu mteule Bi Martha Koome amehimizwa kuzipa kipaumbele kesi za mizozo ya ardhi na mashamba ili kuondoa misongamano kortini, atapovishwa rasmi taji la Rais wa Idara ya Mahakama Nchini (CJ).
Aliyekuwa mbunge mwakilishi wa wanawake Nyeri, Bi Priscilla Nyokabi amesema Jumatatu kesi za mizozo ya mashamba ni kati ya zinazoongoza nchini, na zinapaswa kupewa nafasi ya mbele ili kuzipunguza.
Bi Nyokabi ambaye pia ni wakili alisema CJ Koome atakapochukua mikoba ya uongozi, asaidie kupunguza mrundiko wa kesi za mashamba kortini, zilizokawia muda mrefu.
“Kwa mfano, korti ya mizozo ya ardhi Nyeri haifanyi kazi, na hii ina maana kuwa mizozo ya mashamba imekusanyika. Ninamuomba Martha Koome atakapochukua wadhifa wa uongozi Idara ya Mahakama asaidie kupunguza kesi za mashamba,” akahimiza.
“Kuna wajane wanaoendelea kulilia haki mahakamani baada ya vipande vyao vya ardhi kunyakuliwa. Tunataka malalamishi ya aina hiyo yaamuliwe wapate haki,” Nyokabi ambaye pia ni kamishna wa Tume ya Kitaifa ya Usawa wa Jinsia (NGEC) akasema.
Bi Nyokabi alisema hayo kwenye mahojiano na runinga moja nchini.
Jopokazi la tume ya utendakazi wa Idara ya Mahakama (JSC) liliwahoji wawaniaji wa kiti cha Jaji Mkuu, na kutangaza kumteua Jaji Martha Koome, ambaaye alikuwa miongoni mwa wagombea, baada ya mchakato wa mahojiano kukamilika.
Rais Uhuru Kenyatta aliwasilisha jina la Bi Koome bungeni ili kuhojiwa na kupigwa msasa zaidi.
Endapo bunge litampitisha, kibarua kitasalia kwa Rais Kenyatta kumuidhinisha ili aapishwe rasmi kuchapa kazi kama CJ.
Kiti hicho kilisalia wazi baada ya kustaafu kwa Jaji Mkuu David Maraga, mnamo Desemba 2020.
[ad_2]
Source link