Home » Mashabiki watibua mechi ya EPL kati ya Man-United na Liverpool ugani Old Trafford – Taifa Leo
News

Mashabiki watibua mechi ya EPL kati ya Man-United na Liverpool ugani Old Trafford – Taifa Leo

[ad_1]

Na MASHIRIKA

MCHUANO wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uliokuwa uwakutanishe Manchester United na Liverpool uwanjani Old Trafford mnamo Jumapili uliahirishwa.

Hii ni baada ya takriban mashabiki 200 kujitoma uwanjani na kuandamana dhidi ya familia ya Glazer ambayo inamiliki kikosi hicho kinachojivunia kutwaa ubingwa wa EPL mara 20.

Mechi hiyo ambayo sasa itapigwa katika tarehe mpya itakayotolewa na Shirikisho la Soka la Uingereza (FA), ilikuwa imeratibiwa kuanza saa kumi na mbili jioni.

“Hatua ya kuahirishwa kwa mchuano huo ni maamuzi yaliyofikiwa baada ya kushauriana na maafisa wa polisi, vikosi viwili husika, vinara wa EPL na mamlaka ya usimamizi jijini Manchester,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na EPL.

Kwa mujibu wa ripoti, maafisa wawili wa usalama walijeruhiwa wakati wa maandamano hayo yaliyoandaliwa kulalamikia hatua ya familia ya Glazer kuwatia Man-United kwenye kipute kipya cha European Super League (ESL).

Mbali na Man-United, vikosi vingine vitano vikuu vya EPL vikiwemo Liverpool, Manchester City, Arsenal, Chelsea na Tottenham Hotspur vilikuwa vimekubali kushirikishwa kwenye ESL kabla ya kujiondoa kufuatia hisia kali na malalamiko ya mashabiki na wadau wengine wa soka duniani.

Hii ni mara ya kwanza katika historia kwa mchuano wa EPL kuahirishwa kwa sababu ya maandamano ya mashabiki.

Kabla ya muda ambao mechi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kuwadia, mashabiki walikongamana nje ya uwanja huku wakiteketeza jezi za Man-United.

Licha ya kwamba hakuna mashabiki wanaoruhisiwa kuhudhuria mchuano wowote kwa sasa uwanjani kwa sababu ya janga la corona, baadhi ya mashabiki wa Man-United walipata fursa ya kuingia Old Trafford na kuandamana kabla ya kuondolewa na maafisa wa usalama ila baada ya vurugu, makabiliano na uharibifu wa mali.

Usalama wa kila mshikadau ni muhimu zaidi uwanjani Old Trafford. Tunaelewa na kuheshimu ukubwa wa hisia zilizoonyeshwa na mashabiki wa Man-United. Ni haki yao kuandamana ili kulalamikia kinachowakera. Lakini tusingewaruhusu kwa sababu baadhi yao walikuwa na lengo la kupora, kuzua fujo na pia walikiuka kanuni za kudhibiti maambukizi ya corona,” ikaongeza taarifa ya EPL.

Man-United na Liverpool walikuwa tayari wamefichua vikosi vyao kwa ajili ya mchuano huo kabla ya tukio hilo kushuhudiwa na mechi hatimaye kuahirishwa. Baadhi ya mashabiki wa Man-United walikuwa pia wamekongamana nje ya hoteli ya Lowry ambako wachezaji walikuwa wakikaa kabla ya mchuano huo.

Kufikia sasa, Man-United ya kocha Ole Gunnar Solskjaer inashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL na Man-City wangalitwaa ubingwa wa msimu huu iwapo Liverpool wangeibuka washindi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

[ad_2]

Source link