Home » Muturi atawazwa msemaji Mlima Kenya – Taifa Leo
News

Muturi atawazwa msemaji Mlima Kenya – Taifa Leo

[ad_1]

Na KENNEDY KIMANTHI

SPIKA wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi, Jumamosi alitawazwa kuwa msemaji wa eneo la Mlima Kenya chini ya ulinzi mkali wa polisi.

Hatua hiyo imemuweka katika nafasi nzuri ya kumrithi Rais Uhuru Kenyatta ingawa hajatangaza azima yake kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Bw Muturi aliwasili katika madhababu ya kitamaduni ya Mukurwe wa Nyagathanga, kaunti ya Murang’a akisindikizwa na maafisa wa polisi kufuatia vitisho vilivyokuwa vimetolewa na baadhi ya viongozi kupinga kutawazwa kwake.

Baada ya kuapishwa, anatarajiwa kuunganisha eneo la Mlima na kuhakikisha maslahi ya wakazi wa eneo hili yanawakilishwa katika majukwaa ya kitaifa.

Kabla ya hafla ya Jumamosi, alinukuliwa akisema kwamba yuko tayari kumrithi Rais Kenyatta kama msemaji wa eneo la Mlima Kenya. Mwenyewe alikiri kwamba kutawazwa kwake kutabadilisha mtazamo wa siasa eneo hilo.

“Kumekuwa na tofauti za kimaoni lakini kama eneo, tutadumisha umoja wetu kwa sababu bila hilo hatuwezi kuungwa mkono na maeneo mengine ya nchi. Nitaendelea kushirikiana na Rais Kenyatta na kuunga serikali yake,” alisema.

Kuwepo kwa polisi wengi kulichukuliwa kuwa shughuli hiyo iliyotekelezwa na wazee wa jamii wanaoheshimiwa, ilikuwa na umuhimu mkubwa kwa viongozi na maafisa wa serikali.

Akiwa Spika wa Bunge la kitaifa, Muturi ni mmoja wa maafisa wanaolindwa vikali. Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria alikuwa ametisha kuzuia kutawazwa kwa Bw Muturi.

Mnamo Alhamisi, Bw Iria alisema angewaongoza vijana kuzuia alichotaja kama kuchafua madhabahu takatifu ya jamii ya Agikuyu.

“Huu sio uwanja wa kisiasa bali ni madhabahu. Hata aliyekuwa Rais Mwai Kibaki na Rais Kenyatta hawakujaribu kukufuru eneo hili licha ya kuwa marais na viongozi halisi wa jamii yetu,” Bw Wa Iria alisema.

Hata hivyo baadhi ya viongozi wa eneo la Mlima Kenya akiwemo Gavana wa Meru Kiraitu Murungi waliunga kutawazwa kwa Bw Muturi.

Kulingana na Bw Murungi, eneo la Mlima Kenya linahitaji msemaji wa hadhi ya Bw Muturi ili kudumisha nguvu zake kisiasa.

[ad_2]
Source link