[ad_1]
Na HASSAN MUCHAI
MWANGI Wanjiru almaarufu ‘Malenga Msanifu’ ni mzawa wa Kaunti ya Nyandarua eneo bunge la Ndaragwa.
Yeye ni miongoni mwa vijana wanaodhihirisha upevu wa hali ya juu kwenye ugo wa fasihi andishi haswa utanzi wa mashairi.
Amefanikiwa kuchapisha vitabu kadhaa kikiwemo Medani ya ushairi ambacho kinahakiki utanzu huu wa ushairi kwa lengo la kuwafaa wanafunzi wa shule za sekondari.
Mwangi Wanjiru anasema kwamba kipawa cha utunzi kilianza kudhihirika akiwa shule ya msingi ya Nyonjoro ambapo mwalimu wake wa shule ya msingi Bi Waweru alikipalilia kwa kumshirikisha kwenye tamasha za kuwatumbuiza wageni kwa mashairi mepesi.
“Natumai mwalimu wangu Bi Waweru alibaini nilimiliki kipaji hiki adimu ndiposa akaniteua kila mara kuyaghani mashairi mepesi kuwaburudisha wageni na wazazi kila mara kukiwa na tamasha au hafla yoyote. Sina budi kumshukuru na kumwombea nyota njema maishani mwake,” anasema.
Anasema kuwa alipojiunga na shule ya Sekondari ya Irigithathi iliyoko wilayani Ndaragwa, alielewa kuwa alimiliki kipaji ambacho kilifaa kupaliliwa. Hakuelewa alikuwa na kipaji kwenye fani hii ya lugha hadi alipojiunga na kidato cha kwanza katika shule ya Irigithathi ambako anafunza Kiswahili na somo la dini ya Kikiristo. Walimu wake wa Kiswahili, Bi Ngure na Bw King’ora ndio walioimarisha kipawa chake.
Alipojiunga na kidato cha tatu, alifurahia sana kusoma riwaya ya Kidagaa Kimemwozea ya Ken Walibora. Mwalimu wake alitaka asome kwa sauti kwa niaba ya mwanafunzi wenzake. Jambo hili lilimfanya apende zaidi riwaya hii iliyokuwa na mashairi kadhaa yenye ladha na kuvutia hisia. Alizidi kuimarika kwani kinolewacho hupata.
Miongoni mwa mashairi kwenye riwaya yaliyogusa hisia zake ni haya mawili ambayo alipenda kuyakariri na kunata akilini Mwake hadi leo;
Mkono umeniacha, mwanao kindakindaki
Jitimai limechacha, Amani sifarijiki
Nahisi lau machicha, thamani sithaminiki
Maskini kutwa kucha, natamani kufariki
Tukutane kuko huko
Ulivyonipenda mama, lolote kuniridhia,
Ukajisimamia wima, peke yako kunilea,
Hayo yote tamekoma, niliwa najililia
Machozi kikombe tele
Shairi la huba
Ewe wangu wa ubani, nikuenziye moyoni
Amani nakutamani, kwa huba sizo kifani
Nipe kubali Imani, niwe wako maishani
Katika ndoa ya shani
Mwangi Wanjiru anasema kuwa mashairi haya ya Ken Walibora ni miongoni mwa yale yaliyompa ari na hamu kubwa.
Alianza kutunga akiwa shule ya upili ya Irigithathi.
Zaidi ya hayo, mapenzi yake ya kusoma riwaya za Kiswahili yalimwezesha kujiimarisha kwa ufasaha wa lugha ya Kiswahili. Yeye ni ashiki wa vitabu vya marehemu Ken Walibora, Shabaan bin Robert na Ben R. Mtobwa.
Shairi lake la kwanza kuchapishwa ilikuwa Aprili, 2020, na tangu wakati huo amebahatika kuchapishiwa mengine mengi. Anasema ametunga zaidi ya mashairi mia moja mengi yalkiangazia masuala ya huba.
Kama njia ya kuhamasisha wengine kuenzi na kuelewa ushairi, Mwangi Wanjiru ameandika kitabu cha marudio kwa kwa wanafunzi wa sekondari, kinachohakiki vipashio vyote vya ushairi haswa mashairi ya arudhi.
Hapa anazidi kueleza fahari yake kuhusu ushairi na natija zake, anasema kwamba “Zaidi ya nyimbo, ushairi una raha kwani umepambwa kwa lugha yenye maneno mateule. Kila wakati nikiwa mapumzikoni hupenda kujiburudisha kwa kughani mashairi, aidha niliyoyasarifu au ya malenga wengine kama vile ya Moses Chesire na wengine. ‘’
Anapopatwa na mashaka kimaisha , Wanjiru hujiliwaza kwa kuandika au kuyaghani mashairi. Faida kubwa aliyopata ni kuwa ameukuwa akivuna kutokana diwani yake ‘MEDANI YA USHAIRI’. Kupitia ushairi amejipatia marafiki si haba.
‘’Kwa yote namshukuru Mwenyezi Mungu pamoja na wote walionikuza kwa njia moja au nyingine haswa Mhariri wa makala ya Malumbano kwenye ukurasa wa Jumapili Bwana Hassan Muchai bin Chui, aliyenipandisha ulingoni huu.” Anamalizia.
Hata hivyo, Malenga huyu anayejisabili kwa bidii kufikia mafanikio kama ya watangulizi wake kina Ken Walibora na wengine, anasikitishwa na kupungua kwa washairi nchini Kenya pamoja na kupungua kwa waandishi wa kazi za fasihi. Hata hivyo anawapa hamasa vijana chipukizi wafuate nyayo za watangulizi wao, na kwa kujituma watafikia mafanikio makuu na kufaidi wengi siku zao za halafu.
[ad_2]
Source link