[ad_1]
Na GEOFFREY ANENE
ZIKISALIA siku 17 msimu wa Mbio za Magari Duniani (WRC) 2021 ufike katikati, bingwa mtetezi Sebastien Ogier amezungumzia kwa kina duru hiyo ya Safari Rally akisema madereva watalazimika kubadili mbinu zao ili waponee ukatili wake.
Akizungumza Jumanne na wanahabari na madereva wa Kenya kupitia mtandao wa Zoom, alisema madereva watalazimika kuendesha magari kwa uangalifu mkubwa kutokana na barabara zilizojaa mawe madogomadogo.
Ogier anaamini kuwa Safari Rally, ambayo inarejea kwenye WRC kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002, itakuwa duru ya kusisimua kuendesha magari katika barabara hizo za mawe.Mfaransa huyo yuko katika orodha ya madereva 58 wakiwemo Wakenya watakaowania ubingwa wa Safari Rally mnamo Juni 24-27.
Dereva huyo wa timu ya Toyota Gazoo Racing alisema, “Magari yetu hajakuwa yakishiriki mbio katika hali kama hizo kwa hivyo kitakuwa kitu cha kusisimua. Isitoshe, madereva wengi wa kizazi chetu hawajashiriki mashindano barani Afrika kwa hivyo tunasubiri kwa hamu kubwa mashindano hayo mapya na changamoto.”
Bingwa huyo wa mataji saba ya dunia aliongeza, “Tumekamilisha duru ya Sardinia nchini Italia siku chache zilizopita na tunapumzika nyumbani kabla ya kukuja Kenya kushiriki Safari. Sijui mengi kuhusu duru hiyo, lakini najua kuwa hali ya anga nchini Kenya inaweza kubadilika wakati wowote.
Mvua ikianza kunyesha, mbio zinakuwa ngumu zaidi jinsi ilivyokuwa katika duru ya Mbio za Magari za Afrika za Equator Rally.”Ogier alionya madereva akiwataka wawe waangalifu zaidi na magurudumu yao kutokana na hali ya barabara za mbio za magari za Kenya.
Kwa miaka mingi, Safari Rally imesifika sana kwa kuwa mashindano magumu kabisa duniani.Dereva huyo mwenye umri wa miaka 37 aliongeza kuwa duru ya Kenya itakuwa mashindano katili na yale madereva wa WRC wamezoea na watajaribu kubadilisha mbinu na kuendesha magari kwa uangalifu ili waweze kufanya vizuri.
“Kutokana na habari ninazosikia, barabara za Kenya zina mawe ambayo yanaweza kuwa katili kwa magurudumu. Sio siri kuwa tuna ishu na magurudumu wakati huu. Magurudumu ni muhimu kwa timu zitakazoshiriki Safari ikiwa kweli tunataka kukaa mbali na shida. Barabara zilizo na mawe bila shaka zitasababisha panchari ikiwa madereva hawatakuwa waangalifu,” alisema.
Ogier ni mmoja wa madereva wanane kutoka kote duniani wanaodhaminiwa na kinywaji cha RedBull.Alizoa ushindi wake wa tatu msimu huu aliposhinda duru ya Sardinia nchini Italia wikendi iliyopita baada ya kutamba nchini Monaco na Croatia.Ogier pia alifichua kuwa anapenda sana duru mpya na changamoto mpya.
“Kile nimepanda katika miaka 15 nimekuwa katika mashindano ya mbio za magari ni kushiriki mikondo mipya. Kwa hivyo, nina hamu kubwa kuja Kenya kwa mara ya kwanza. Inafurahisha kuona kuwa mashabiki Kenya wameonyesha wanatamani sana kuona mashindano ya Safari Rally yakirejea WRC baada ya miaka 19,” alisema.
[ad_2]
Source link