[ad_1]
Na GEOFFREY ANENE
WAAJIRI wapya wa mshambuliaji Mkenya Ismael Dunga, Sagan Tosu wameanza maandalizi ya msimu mpya kwa kuchabanga Okinawa SV 3-1 katika uwanja wa Zampa Misaki Ball Park, Jumatano.
Sagan, ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Japan (J1 League), imekita kambi Okinawa kuanzia Januari 25 hadi Februari 8.
Inapanga kuwa na kambi ya mwisho katika eneo hilo Februari 9-13 kabla ya msimu 2021 kung’oa nanga Februari 26.
Katika mchuano huo wa mazoezi dhidi ya timu hiyo kutoka ligi ya daraja ya tano, ambao uligawanywa katika vipindi vitatu vya dakika 30 kila kimoja, Sagan ilitoka 1-1 katika mechi ya kwanza, 0-0 katika mechi ya pili kabla ya kutamba 2-0 katika kipindi cha mwisho. Mechi hizo zilisakatwa bila mashabiki kutokana na janga la virusi vya corona.
Dunga,27, alijiunga na Sagan mnamo Januari 25 kutoka Vllaznia inayoshiriki Ligi Kuu ya Albania kwa ada inayoaminika kuwa Sh9.3 milioni. Kandarasi yake itakatika Januari 31, 2022.
Haikubainika mara moja kama Dunga alishiriki michuano hiyo dhidi ya Okinawa kwa sababu sheria za serikali ya Japan za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona zinahitaji wageni kutoka nchi 53 ya Bara Ulaya ikiwemo Albania kuingia karantini mara tu wanapowasili kwa siku 14. Klabu yake pia haijachapisha orodha ya wachezaji walioshiriki mazoezi hayo wala picha zao pamoja na wafungaji wa mabao.
Sagan itaanza kampeni ya Ligi Kuu ambayo imeongezwa timu mbili na kufikia timu 20 msimu huu, dhidi ya Shonan Bellmare mnamo Februari 27 ugenini.
Timu ya Sagan ilikamilisha msimu uliopita katika nafasi ya 13 kwa alama 36, tisa zaidi ya Shonan iliyovuta mkia.
Mshambuliaji Mkenya Michael ‘Engineer’ Olunga aliibuka mfungaji bora pamoja na kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2020 kwenye ligi hiyo ya Japan baada ya kuongoza Kashiwa Reysol kukamilisha kampeni katika nafasi ya saba. Olunga alijiunga na mabingwa wa Ligi Kuu ya Qatar (QSL) Al Duhail mnamo Januari 12.
[ad_2]
Source link