Home » Uhuru aangusha minofu kwa Raila – Taifa Leo
News

Uhuru aangusha minofu kwa Raila – Taifa Leo

[ad_1]

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta mnamo Jumapili alianza kuangushia kinara wa ODM Raila Odinga minofu ya handisheki kwa kuzindua miradi kadhaa ya maendeleo katika ngome ya kisiasa ya Bw Odinga.

Kwenye ziara yake eneo la Nyanza inayoashiria kilele cha handisheki kati yake na Bw Odinga, Rais Kenyatta anatazamiwa kuendelea kuzindua miradi mikuu, ukiwemo ule wa Bandari ya Kisumu.

Alipowasili Kisumu, Jumapili saa tisa alasiri, Rais Kenyatta alielekea moja kwa moja hadi Kaunti ya Siaya ambako ni nyumbani kwa Bw Odinga, ambapo alizindua miradi ya maji na unadhifishaji.

Reli ya Nakuru-Kisumu ilikuwa miongoni mwa miradi aliyotarajiwa kuzindua lakini iliahirishwa kutokana na kutokuwa tayari.

Katika hatua itakayopiga jeki pakubwa eneo hilo kiuchumi, Rais anatazamiwa kuzindua Bandari ya Kisumu yenye thamani ya Sh3 bilioni leo hii, na kufikisha kikomo wasiwasi wa miezi mingi miongoni mwa wakazi kuhusu mradi huo mkuu.

Rais atazindua rasmi treni ya MV Uhuru itakayokuwa na mabehewa 22 yatakayoibeba lita 50,000 za petroli kila moja kati ya Jinja-Uganda.

Jumapili alipotua jijini Kisumu, kabla ya Maadhimisho ya 58 ya Sikukuu ya Madaraka Jumanne, alipokelewa kwa mbwembwe ikiwemo kusafishiwa barabara.

Maadhimisho ya Sikukuu ya Madaraka mwaka huu ni spesheli na tukio kuu, ikizingatiwa ni mara ya kwanza kwa sherehe za Sikukuu hiyo ya Kitaifa kuwahi kuandaliwa Kisumu tangu Kenya ilipoanza kujitawala 1963.

Kama sehemu ya matayarisho ya kupamba mji huo kumpokea Kiongozi wa Taifa na viongozi wengine mashuhuri, maafisa wa Idara ya Zima Moto walionekana na mifereji ya maji wakisafisha barabara ya Oginga Odinga.

Maafisa hao walitumia mitambo ya zima moto kuondoa vumbi na takataka kwenye barabara hiyo.

Wakazi waliokuwa na hamu ya kumwona Rais Uhuru walikusanyika kandokando ya barabara kuu katika mji huo ulio kando na Ziwa Victoria, wakisubiri kuwasili kwa msafara wa rais.

Mamia ya wakazi walifurika katika maeneo ya Riat na Kicomi huku wengine kadhaa wakisongamana kwenye barabara inayoelekea hoteli maarufu ya Kisumu State Lodge, kwenye barabara kuu ya Jomo Kenyatta.

Wengine walikusanyika kandokando ya Barabara Kuu ya Busia ambapo Rais alitazamiwa kuzindua reli inayounganisha Kisumu na Nakuru.

Hata hivyo, kinyume na matarajio ya wengi, ziara ya kwanza ya Rais hadi Kisumu kwa kutumia treni ilifutiliwa mbali ghafla katika dakika ya mwisho kutokana na kile Msemaji wa Rais Kanze Dena alitaja kama “sababu zisizoepukika.”

Kulingana na tangazo la awali, Rais Uhuru na Kiongozi wa ODM Raila Odinga walitarajiwa kuabiri treni ya MGR mjini Nakuru jana asubuhi kabla ya Sikukuu ya Madaraka na kusafiri nayo hadi Kisumu, kama ishara ya reli hiyo kurejelea shughuli zake.

Kilele cha ziara hiyo ya siku tatu ya Rais mjini Kisumu kitakuwa maadhimisho ya sherehe za Sikukuu ya Madaraka zitakazofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Jomo Kenyatta, eneo la Mamboleo, ambazo pia zitahudhuriwa na Rais wa Burundi Evariste Ndashimiye kama mgeni wa heshima.

CAROLINE WAFULA, RUSHDIE OUDIA na MARY WANGARI

[ad_2]

Source link