[ad_1]
Na WANDERI KAMAU
NI wazi sasa kwamba Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi, ndiye mrithi rasmi wa Rais Uhuru Kenyatta kama msemaji wa ukanda wa Mlima Kenya, baada ya taratibu za kitamaduni kumtawaza kukamilika.
Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, Bw Muturi amekuwa faraghani kwa siku nane mfululizo, ambapo amekuwa akifanyiwa matambiko maalum ya kitamaduni na wazee ili kuhakikisha “hana doa lolote.”
Kwa mujibu wa wazee ambao wamekuwa wakimwangalia na kumpa ushauri, taratibu hizo ni za kipekee na huwa zinafanyiwa tu mtu anayeonekana kuwa na uwezo wa “kuziongoza” na “kuzikomboa” jamii.
Wazee hao wanatoka katika jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (GEMA).
Kwenye mahojiano na Jamvi la Siasa, wazee hao walisema kuwa taratibu anazopitishwa Bw Muturi ni za kipekee, na ni viongozi wachache sana kutoka ukanda huo wamewahi kufanyiwa hivyo tangu nchi ilipojinyakulia uhuru mnamo 1963.
Utaratibu huo unajiri miezi miwili baada ya Bw Muturi kuidhinishwa kuwa msemaji wa ukanda huo na wazee kutoka jamii ya Ameru, almaarufu kama Njuri Ncheke katika eneo la kitamaduni la Nchiru, Kaunti ya Meru.
Kwa mujibu wa wazee na wadadisi wa masuala ya kitamaduni wa jamii za Gema, ni Mzee Jomo Kenyatta, Rais Mstaafu Mwai Kibaki na Rais Uhuru Kenyatta pekee waliofanyiwa matambiko kama hayo.
“Huu ni utaratibu muhimu na wenye uzito mwingi mno. Unawahusisha wazee wa jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru ili kuhakikisha kiongozi anayetawazwa atakuwa na uwezo wa kuziunganisha jamii zote zilizo katika ukanda huo,” akasema mzee Phares Ruteere, aliye miongoni mwa wazee wanaohusika katika taratibu hizo.
Upeo wa “uidhinishaji” wa Bw Muturi ulikuwa Jumamosi ambapo alipelekwa katika eneo la Mukurwe wa Nyagathanga, katika Kaunti ya Murang’a, ambako jamii ya Agikuyu inaamini kuwa usuli wake unapatikana.
Kwa mujibu wa Prof Peter Kagwanja, ambaye pia ni miongoni mwa wazee ambao wamekuwa wakihusika katika shughuli hizo, uamuzi wa kumtawaza Bw Muturi unatokana na tajriba yake pana katika uongozi na uzalendo mkubwa ambao ameonyesha katika kutetea maslahi ya wenyeji wa Mlima Kenya kama kiongozi katika ngazi ya kitaifa.
“Ikiwa ataidhinishwa, Bw Muturi atakuwa na nafasi nzuri sana ya kulitetea eneo hili, kwani ametangamana na wabunge kutoka kila sehemu nchini tangu 2013. Kwa tajriba hiyo, ana ufahamu mkubwa kuhusu njia atakazotumia kuhakikisha eneo hili limeungana kisiasa na kiuchumi na maeneo mengine nchini,” akasema Prof Kagwanja.
Wadadisi wanasema sababu nyingine inayomfanya Bw Muturi kupendelewa ni kwa sababu yuko katika nafasi nzuri ya “kuzima” uhasama ambao umekuwepo kati ya jamii hizo, ambapo jamii ya Agikuyu imekuwa ikilaumiwa na Ameru, Aembu na Mbeere kwa “kukwamilia” katika uongozi wa ukanda huo.
Mzee Kenyatta, Bw Kibaki na Rais Kenyatta ndio wamekuwa viongozi na wasemaji wa kisiasa katika eneo hilo. Wadadisi wanasema uwepo wa wazee kutoka jamii hizo tatu kubwa unaonyesha kuna muafaka uliopo kati ya mabwanyenye na viongozi wa kisiasa katika ukanda huo.
“Kimsingi, ilitarajiwa kwamba hatua hiyo ingepata pingamizi kubwa kutoka kwa viongozi na watu wenye ushawishi mkubwa katika eneo hilo. Hata hivyo, kimya kilichopo ni ishara kwamba kuna taratibu za kichinichini zilizoendeshwa kuzima migawanyiko ambayo huenda ikaibuka,” asema Dkt Godfrey Sang’ ambaye ni mchanganuzi wa siasa . Baadhi ya viongozi ambao wametangaza kumuunga mkono Muturi ni Gavana Kiraitu Murungi (Meru), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi) na Martin Wambora (Embu). Hata hivyo, magavana wengine kutoka eneo la Kati wamebaki kimya.
Lakini Ijumaa, baadhi yao walijitokeza na kusema kuwa uidhinishaji wa Bw Muturi haukuwahusisha wenyeji wote wa Mlima Kenya, hivyo hatua hiyo haimaanishi kwamba watamuunga mkono.
Gavana Anne Waiguru (Kirinyaga) alisema mchakato huo ni muhimu sana, hivyo lazima umhusishe kila mtu.
Alikosoa vikali wanaouendesha, akiwataja kuwa wenye njama za kutaka “kumpindua kisiasa” Rais Uhuru Kenyatta kama kiongozi na msemaji wa kisiasa wa ukanda huo.
Kauli kama hiyo ilitolewa na Gavana Mwangi wa Iria (Murang’a), aliyemtaja Bw Muturi kuwa “chaguo la wachache.”
Mbunge Rigathi Gachagua (Mathira) alimtahadharisha Bw Muturi awe mwangalifu, asije akadanganywa na viongozi na wazee wachache wanaojitakia makuu.
“Bw Muturi ni rafiki yangu wa muda mrefu. Kama rafiki yake, ningetaka kumrai kuwaendea wananchi moja kwa moja ikiwa anataka kuchaguliwa kuhudumu katika nafasi yoyote ya uongozi. Anajidanganya kuwategemea wazee kumtawaza,” akasema Bw Gachagua.
Kufikia sasa, Rais Kenyatta hajazungumzia lolote kuhusu uidhinishwaji huo, ijapokuwa wadadisi wanataja kimya chake kuwa “mbinu ya kuondoa dhana kwamba Bw Muturi ni mradi wake wa kisiasa.”
“Ilivyo sasa, Rais Kenyatta anakabiliwa na upinzani wa kisiasa katika eneo la Kati. Kimya chake ni njia ya kuondoa hisia zozote kuwa anahusika kumjenga Bw Muturi kisiasa,” asema Dkt Sang’.
[ad_2]
Source link