[ad_1]
Na BENSON MATHEKA
KINARA wa chama cha Amani National Congress (ANC) Wycliffe Musalia Mudavadi, anaweza kuwa mmoja wa wanasiasa wachache wanaosema ukweli wa hali halisi ya uchumi na utawala nchini.
Hata hivyo, wadadisi wanasema amezoea kudandia nyadhifa za uongozi badala ya kujitokeza kuzipigania kwa nguvu pamoja na kutetea maslahi ya Wakenya, wakiongeza kuwa kuwa Bw Mudavadi ana sifa zote za kuwa kiongozi bora lakini anachokosa ni ujasiri na mvuto wa kisiasa.
Bw Mudavadi alijiunga na siasa 1989 alipochaguliwa kuwakilisha eneobunge la Sabatia, Kaunti ya Vihiga, kufuatia kifo cha baba yake Moses Mudavadi, ambaye alikuwa mbabe wa siasa za eneo la Magharibi. Alisaidiwa katika uchaguzi huo na aliyekuwa rais, marehemu Daniel Moi ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa baba yake.
“Musalia alitumia urafiki wa baba yake na Moi kujiunga na siasa. Ni Moi aliyemshika mkono na kumlea kisiasa,” asema mdadisi wa siasa Tom Maosa.
Anasema tangu wakati huo, Bw Mudavadi hajawahi kujisimamisha kivyake kisiasa akafaulu, na badala yake amekuwa akitegemea umaarufu wa wanasiasa wengine kuchaguliwa.
Kwenye chaguzi za 1992 na 1997, Musalia alichaguliwa kwa tiketi ya Kanu kutokana na umaarufu wa Mzee Moi. Umaarufu wa Kanu ulipofifia kwenye uchaguzi mkuu wa 2002 Moi alipokuwa akistaafu, Bw Mudavadi alipoteza kiti chake cha ubunge cha Sabatia. Wakati wa uchaguzi huo, alikuwa makamu wa rais na mgombea mwenza wa mwaniaji urais wa Kanu, Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa chaguo la Moi.
“Ilibidi akae kwenye baridi hadi 2005 alipojiunga na Raila Odinga kupinga kura ya maamuzi ya katiba. Alikwamilia kwa Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2007 akiwa mgombea mwenza wake, na katika serikali ya muungano akateuliwa naibu waziri mkuu,” asema mchanganuzi wa siasa Raymond Kongo.
Kuachwa Kwenye Mataa
Kwenye uchaguzi mkuu wa 2013, Musalia alijitenga na Bw Odinga na kujiunga na chama cha United Democratic Party (UDP) alichotumia kugombea urais. Baadhi ya wadadisi wa siasa wanasema wakati huo alitarajia kunufaika na uungwaji mkono kutoka kwa Rais Kenyatta, ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).
“Kulikuwa na duru za kuaminika kwamba Uhuru alikuwa amezungumza na Mudavadi amuunge mkono kugombea urais kufuatia utata uliogubika kesi iliyomkabili ICC, lakini baada ya kushauriana kwa upana, Uhuru aliungana na Ruto,” asema Bw Kongo.
Rais Kenyatta baadaye alikiri kwamba alikuwa amepanga kumuunga mkono Bw Mudavadi lakini akabadili nia.
Kwenye uchaguzi huo wa 2013, Bw Mudavadi aligombea urais kwa tiketi ya UDP na akaibuka wa tatu nyuma ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.
Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, Bw Mudavadi aliunda chama cha ANC na akapata nguvu mpya Katibu Mkuu wa Muungano wa Wyama vya Wafanyakazi, Francis Atwoli alipomtawaza msemaji wa Waluhya na kumtwika jukumu la kupatia jamii hiyo mwelekeo wa kisiasa.
Aliungana na kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula, Raila Odinga wa chama cha ODM na Kalonzo Musyoka wa Wiper kuunda muungano wa NASA kukabili Jubilee.
Kulingana na mkataba wa maelewano wa NASA, Bw Odinga angepeperusha bendera ya muungano huo kwa miaka mitano pekee na kuachia vinara wenzake kuamua mgombea urais wao kwenye uchaguzi mkuu wa 2022. Hii ingempatia Bw Musalia nafasi ya kutegemea umaarufu wa Bw Odinga iwapo angeteuliwa kupeperusha bendera ya muungano huo.
Hata hivyo, mambo yalibadilika Bw Odinga aliposikizana na Rais Kenyatta na kumuacha Bw Mudavadi na vinara wenzake kwenye mataa hadi BBI ikampa matumaini mapya.
“Musalia alijikokota kuunga mkono BBI hadi alipong’amua kwamba kuna uwezekano wa Rais Kenyatta kumuunga mkono kugombea urais baada ya mchakato huo kufaulu, au apate moja kati ya nyadhifa za uongozi zitakazobuniwa katiba ikifanyiwa mageuzi,” aeleza Bw Kongo.
Bw Mudavadi pia amekuwa akifurahia kauli ya Rais Kenyatta kwamba wakati umefika kwa jamii nyingine kuongoza mbali na Wakikuyu na Wakalenjin, na wadadisi wanasema ni kwa sababu hii anadhani anaweza kunufaika.
[ad_2]
Source link