[ad_1]
Na SAMMY KIMATU
MTOTO wa umri wa mwaka mmoja na mwezi moja alifariki Jumatano alipokanyagwa na lori katika mtaa mmoja wa mabanda Kaunti ya Nairobi.
Kutokana na kisa hicho, wakazi waliokuwa na hasira walifunga barabara katika eneo la ajali hiyo wakiandamana.
Ilibidi maafaisa wa polisi wa kupambana na ghasia kuwasili na kuwatawanya waandamanaji kwa kutumia gesi ya machozi.
Kisa hiki kilitokea katika eneo la Lengo katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba ulioko kaunti ndogo ya Starehe.
Kwa mujibu wa kiongozi wa vijana eneo la South B, Bw Rotrigues Lunalo, dereva aliyesababisha maafa hayo alikuwa amepeleka pombe aina ya Keg katika depo moja ilioko mtaani huo.
Aliongeza kwamba mtoto huyo alikuwa ameketi juu ya kiti nje ya duka lao huku mamamke aliyekuwa naye akimuacha nje peke yaken na kuingia ndani ya duka kuhudumia mteja. Kisha lori la pombe likawasili na ndipo mtoto aliposikia mngurumo wa gari, alianguka chini ya lori na kukanyangwa mara hio.
“Mtoto aliachwa na mama yake nje ya duka akikalia kiti alipoenda kuuzia mteja bidhaa dukani.
Mtoto alishtuliwa na mngurumo wa lori ndiposa akaanguka chini na kukanyangwa,’’ Bw lunalo akasema.
Wakazi walighadhabishwa na tukio hilo na kuanzisha maandamano mara moja.
Shughuli zilisimama kwa muda mtaani na barabarani kwa saa nne polisi wakikabiliana na waandamanaji.
Barabara ya Busia ilikuwa haipitiki baada ya vijana kuifunga sawia na kufunga barabara ya Sigei inayoingia mtaani huo.
Polisi walilazimika kurusha vitoza machozi na kupiga risasi hewani ili kuwatawanya.

Baadaye, mbunge wa eneo hilo, Bw Charles Njagua Kanyi aliwasili, akawahotubia na kuwatuliza waandamanaji.
“Hakuna haja ya nyinyi kuwa na wazo la kuchoma gari. Ni vyema mnipatie viongozi watano ili tuende hadi kituoni cha polisi kupeleka malalamishi yetu,” mbunge Janguar akasema.
Naibu kamanda wa polisi eneo la Makadara, Bi Judith Nyongesa alithibitisha dereva wa lori alikamatwa na kufungiwa kituoni cha polisi cha Industrial Area. Vile vile, Bi Nyongesa aliongeza kwamba mshukiwa atafikisha kortini leo.
Kadhalika, alitoa wito kwa wazazi kumakinika kuwatunza watoto wao wanapokuwa nyumbani ili kuepukana na ajali kama ya Jumatano.
Aliwaomba wenyeji kutosababisha fujo au ghasia wakati wa tukio kama lile na badala yake wadumishe amani na kutafuta suluhisho kwa njia ya amani badala ya kuchukua sheria mikononi mwao.
“Nawaambia wazazi ni lazima watunze watoto wakiwa nyumbani wasije wakapatwa na mambo mambaya wakiwa peke yao. Kwa vijana, hakuna haja ya kuzua rabsha, kuna taratibu za kutumia kwa mujibu wa sheria kutatua mambo badala ya kusababisha machafuko na uharibifu wa mali wakati kuna maandamano,’’ Bi Nyongesa akasema.
Alisema marehemu alitambuliwa kwa jina Destiny Makavi, msichana wa umri wa mwaka mmoja na mwezi mmoja.
Aliongeza kwamba watu wakiandamana huwa wanahitilafiana na uchunguzi wa posisi ambapo mambo kama ushahidi huvurugika wakati wa kesi za aina hiyo.
[ad_2]
Source link