[ad_1]
Na KALUME KAZUNGU
WAVUVI katika kisiwa cha Lamu wanaiomba serikali kuingilia kati na kuwasaidia kukomboa ardhi yao ya maegesho inayodaiwa kunyakuliwa na mabwanyenye.
Ardhi hiyo ya ekari moja ambayo ndiyo maegesho ya pekee ya wavuvi iliyosalia mjini Lamu inapatikana karibu na eneo la KenGen.
Mwenyekiti wa kikundi cha wavuvi mjini Lamu, Bw Abubakar Twalib, alilalamika kuwa licha ya ardhi hiyo kutambulika kuwa ya umma na ambayo imekuwa ikitumika kama maegesho ya wavuvi tangu ukoloni, inashangaza kwamba mabwenyenye wamejitokeza kudai umiliki wake.
Ukuta tayari umejengwa kwenye maegesho hayo, hivyo kuwazuia wavuvi kuitumia.
“Tulipozaliwa tulipata wazee wetu tayari wakitumia maegesho haya. Tunavyojua ni kwamba ardhi ni ya umma na ilitengewa wavuvi tangu ukoloni. Tumeshangazwa na hatua ya mabwenyenye watatu ambao wamejitokeza kudai umiliki wa kipande hicho cha ardhii,” akasema Bw Twalib.

Naibu Gavana wa Lamu, Abdulhakim Aboud, ambaye pia ni Waziri wa Uvuvi eneo hilo, alisema mikakati inaendelea kwenye ofisi yake ili kuona kwamba maegesho ya wavuvi kote Lamu yanalindwa kupitia utoaji wa hatimiliki.Alisema aliwasiliana na Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) mwezi uliopita na maafisa wakatumwa Lamu kukagua ardhi hizo kwa maandalizi ya kutoa hatimiliki.
“Wavuvi wasiwe na shaka. Tunatarajia shughuli ya kutoa hatimiliki kwa maegesho ya wavuvi kote Lamu ianze wakati wowote,” akasema Bw Aboud.
Omar Sharif ambaye ni mvuvi wa tangu jadi Lamu alisema ukosefu wa hatimiliki za vipande vingi vya ardhi zinazotumika kama maegesho ya wavuvi kumetoa mwanya mwafaka wa mabwenyenye kuzilenga na kuzinyakua ardhi hizo kiholela.
Mbali na maegesho ya wavuvi yanayodaiwa kunyakuliwa kisiwani Lamu, wavuvi pia wamekuwa wakidai kuwa maegesho iliyoko eneo la Tenewi ilinyakuliwa.
Bw Sharif alisema kuendelea kunyakuliwa kwa maegesho ya wavuvi kumechangia kukosa kupanuka kwa sekta ya uvuvi na samaki kote Lamu.
[ad_2]
Source link