[ad_1]
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanawake ya Kenya maarufu Lionesses imeanza kambi ya mazoezi na mashindano ya mwaliko ya Tunisia kwa kishindo Jumamosi.
Lionesses A imechabanga Madagascar A pembamba 14-12 nayo Lionesses B ikararua Madagascar B 19-0 mjini Tunis.
Madagascar ilizoa ushindi muhimu dhidi ya wenyeji baada ya timu yake ya A kuchapa Tunisia A 12-5 nayo ile ya B ikapepeta Tunisia B 19-10.
Timu hizo zilipimwa virusi vya corona kabla ya kuruhusiwa kuanza kambi hiyo Aprili 30 itakayokamilika Mei 8. Lionesses, ambayo iliwasili Tunis mnamo Aprili 30, inajiandaa kwa michezo ya Olimpiki itakayofanyika mjini Tokyo nchini Japan mnamo Julai 23 hadi Agosti 8 mwaka huu.
Vipusa wa kocha Felix Oloo walishiriki mazoezi na mashindano ya mwaliko nchini Uhispania mwezi Februari na nchini Milki za Kiarabi mwezi Machi.
Wako katika orodha ya mataifa 10 yaliyofuzu kwa Olimpiki. Mataifa mengine yaliyojikatia tiketi ni Japan (wenyeji), New Zealand, Amerika, Canada, Australia, Brazil, Uingereza, Fiji na Uchina.
Tunisia na Madagascar wako katika mashindano ya mwisho ya kuingia Olimpiki yatakayoleta pamoja mataifa 12 nchini Monaco mnamo Juni 19-20.
[ad_2]
Source link









