Home » ‘Kiwango cha maambukizi ya corona kinaendelea kushuka’ – Taifa Leo
News

‘Kiwango cha maambukizi ya corona kinaendelea kushuka’ – Taifa Leo

[ad_1]

Na CHARLES WASONGA

KIWANGO cha maambukizi ya Covid-19 nchini Jumatatu kiliendelea kuwa cha chini baada ya Kenya kuandikisha kiwango cha asilimia 5.3.

Kiwango hiki ni cha juu kidogo ikilinganishwa na kile cha asilimia 4.7 kilichoripotiwa Jumapili.

Kulingana na taarifa kutoka kwa Wizara ya Afya, Jumatatu, idadi ya maambukizi mapya 88 ya virusi vya corona kutokana na sampuli 1,668 zilizopimwa ndani ya saa 24.

Idadi hiyo sasa inafikisha 170,735 idadi jumla ya maambukizi tangu mwaka 2020 baada ya jumla ya sampuli 1,811,558 kupimwa.

Idadi ya vifo vipya kutokana na corona ilikuwa 15 ambazo ziliripotiwa katika vituo mbalimbali vya afya katika tarehe mbalimbali tangu mwezi wa Aprili.

Kwa hivyo, idadi jumla ya vifo nchini Kenya imepanda hadi 3,172.

“Habari njema ni kwamba jumla ya wagonjwa 71 wa corona walipona kutokana na ugonjwa huo; 64 wakiwa ni wale ambao walikuwa wakitunzwa nyumbani na saba wakiwa ni wale ambao walikuwa wamelazwa katika hospitali mbalimbali,” ikasema taarifa hiyo ambayo ilitiwa saini na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Idadi jumla ya wagonjwa wa Covid-19 waliopona sasa imetimu 116,847.

Na 84,896 kati yao ni wale waliokuwa wanahudumiwa nyumbani huku 31,951 wakiwa ni wale waliokuwa wamelazwa katika vituo mbalimbali vya afya.

Vile vile, jumla ya wagonjwa 1,237 wa corona wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini huku 4,661 wakiuguzwa nyumbani.

Nao wagonjwa 93 wako katika vyumba vya kuwahudumia wagonjwa mahututi, 21 kati yao wakiwekewa mitambo ya kuwasaidia kupumua. Wengine 55 wanaongezwa oksijeni kwa njia ya kawaida huku 17 wakichunguzwa kwa karibu.

Kwa mujibu wa utoaji chanjo, jumla ya watu 969,489 wamepewa chanjo hiyo dhidi ya Covid-19 kote nchini kufikia Jumatatu.

Vile vile, ni watu 203 pekee ambao wamepewa dosi ya pili ya chanjo ya kuzuia ugonjwa wa Covid-19.

Miongoni mwao ni wahudumu wa afya 160, maafisa wa usalama 17, wanne ni wenye umri wa miaka 58 kwenda juu ilhali wengine 22 wanatoka makundi mbalimbali ya wananchi.

[ad_2]
Source link