[ad_1]
Na MASHIRIKA
LICHA ya kucheza kwa zaidi ya dakika 80 wakiwa na wanasoka 10 pekee uwanjani, kikosi cha Southampton kiliwalazimishia Leicester City sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Aprili 30, 2021.
Matokeo hayo yaliyaweka Leicester ya kocha Brendan Rodgers katika hatari ya kutokamilisha kampeni za muhula huu ndani ya orodha ya nne-bora na hivyo kukosa fursa ya kunogesha kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.
Beki Jannick Vestergaard alifurushwa uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu na refa Robert Jones katika dakika ya 10 kwa kosa la kumchezea visivyo fowadi Jamie Vardy.
Tukio hilo liliwachochea Southampton almaarufu The Saints kuibana sana safu yao ya ulinzi huku Leicester nao wakilibisha lango la wenyeji wao kwa kipindi kirefu. Ingawa hivyo, ni Southampton ya kocha Ralph Hasenhuttl ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuona lango la wapinzani kupitia bao la James Ward-Prowse katika dakika ya 61.
Goli hilo lilitokana na penalti ambayo Southampton walipokezwa baada ya fowadi raia wa Nigeria, Kelechi Iheanacho kumchezea visivyo Stuart Armstrong ndani ya kijisanduku.
Jonny Evans alisawazishia Leicester kunako dakika ya 68 baada ya kukamilisha krosi ya Iheanacho aliyeshirikiana vilivyo na Vardy kumshughulisha kipa Alex McCarthy wa Southampton.
Matokeo hayo yalidumisha Leicester katika nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 63, tano nyuma ya Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora. Kikosi hicho cha kocha Rodgers sasa kiko katika hatari ya kupitwa na West Ham United, Liverpool, Tottenham Hotspur na Everton ambao pia wanafukuzia fursa ya kumaliza kampeni za EPL muhula huu ndani ya mduara wa nne-bora.
Southampton kwa upande wao wanashikilia nafasi ya 14 kwa pointi 37 huku pengo la alama 10 likitamalaki kati yao na Fulham ambao kwa pamoja na West Bromwich Albion, wako katika hatari ya kuteremshwa ngazi msimu huu baada ya Sheffield United.
Huku Leicester wakiwaalika Newcastle United katika mchuano wao ujao wa EPL mnamo Mei 7, 2021 ugani King Power, Southampton watakuwa wageni wa Liverpool siku moja baadaye uwanjani Anfield.
Mechi dhidi ya Newcastle ndiyo ya pekee inayotarajiwa kuwa mteremko kwa Leicester watakaofunga msimu kwa kucheza na Chelsea katika fainali ya Kombe la FA na kupepetana na Manchester United, Chelsea na Tottenham katika michuano mitatu ya mwisho ligini.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO
[ad_2]
Source link









