Home » Majumba 2,000 ya kisasa kujengwa Gatanga na Juja – Taifa Leo
News

Majumba 2,000 ya kisasa kujengwa Gatanga na Juja – Taifa Leo

[ad_1]

Na LAWRENCE ONGARO

KAMPUNI ya Kamuthi Housing Co-operative Society, kwa ushirikiano na kampuni ya ujenzi ya Fourteen Trees pamoja na benki ya Co-operative, inakusudia kuwekeza kwa mradi wa ujenzi wa majumba ya watu kumiliki.

Mkurugenzi wa Kamuthi Housing Co-operative Society, Bw Murakaru Gatheru, alieleza kuwa lengo lao kuu ni kuwahimiza wananchi popote walipo wanunue na kumiliki nyumba zao wenyewe.

Alieleza tayari wametenga jumla ekari 400 eneo la Soya Dam lililoko Gatanga, na Juja, kwa lengo la kujenga majumba 2,000 kwa wateja wapatao 10,000.

“Tunaendeleza mojawapo ya Ajenda Nne muhimu za serikali kwa kujenga nyumba za kuishi zitakazomilikiwa na wanunuzi. Mpango huo ni wa kunufaisha wananchi wengi,” alifafanua Bw Gatheru.

Alisema kampuni hiyo ya Kamuthi Housing, na washikadau wengine walioweka mkataba nao, watahakikisha wanajenga nyumba za kisasa zitakazowanufaisha wamiliki wake.

Bw Gatheru alitoa wito kwa kila mwananchi mwenye kujituma afanye hima kuhakikisha nyumba hizo zikikamilika anapata fursa ya kumiliki angalau moja ili kuishi maisha yasiyo ya kulipa kodi ya kila mwezi.

Kampuni hiyo inajihusisha na ujenzi wa nyumba za bei nafuu za kati ya Sh3.5 na Sh7 milioni.

Alithibitisha kuwa kwa muda wa mwaka mmoja ujao watakuwa wamepiga hatua kubwa kwa ujenzi wa nyumba hizo zitakazokuwa za kisasa.

Bw Gatheru alisema tayari wateja wengi wamejitolea kuwekeza katika ununuzi wa majumba hayo.

“Tayari tumepata wateja wengi ambao wamejitolea kuwa wamiliki wa nyumba hizi zitakapokamilika. Hiyo ni hatua nzuri kwa wale wanaoelewa umuhimu wa kuwa na nyumba zao kibinafsi,” akisema mkurugenzi hiyo.

Alisema uwekezaji wa kumiliki nyumba za kibinafsi umechukua mwelekeo mpya kwani watu wengi wakati huu wamekuja kuelewa umuhimu wa kumiliki nyumba zao.

[ad_2]
Source link