Home » Kocha Nuno Espirito Santo kuvunja ndoa kati yake na Wolves mwishoni mwa msimu huu – Taifa Leo
News

Kocha Nuno Espirito Santo kuvunja ndoa kati yake na Wolves mwishoni mwa msimu huu – Taifa Leo

[ad_1]

Na MASHIRIKA

KOCHA Nuno Espirito Santo ataagana rasmi na kikosi cha Wolves mwishoni mwa msimu huu.

Mkufunzi huyo raia wa Ureno mwenye umri wa miaka 47 alianza kudhibiti mikoba ya Wolves mnamo 2017 baada ya kukatiza uhusiano na FC Porto ya Ligi Kuu ya Ureno. Alishindia Wolves taji la Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) katika msimu wake wa kwanza uwanjani Molineux.

Katika kipindi cha misimu miwili iliyopita (2018-19 na 2019-20), Wolves walikamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya saba jedwalini.

Ufanisi huo ulichochea wasimamizi wa Wolves kurefusha mkataba wa kocha huyo kwa miaka mitatu zaidi mnamo Septemba 2020 na yalikuwa matarajio yao kwamba angeendelea kuhudumu ugani Molineux hadi Septemba 2023.

“Tuliyafikia mengi ya malengo yetu kama kikosi. Tulifanya hivyo kwa kujitolea. Tuliongozwa na mapenzi ya dhati na tulifanya hivyo kwa ushirikiano mkubwa,” akasema Nuno.

Kufikia sasa, Wolves wanashikilia nafasi ya 12 kwenye msimamo wa jedwali la EPL na watafunga rasmi kampeni za kipute hicho dhidi ya Manchester United uwanjani Molineux mnamo Mei 23, 2021.

“Tangu nilipotua ugani Compton ambao ni uwanja wetu wa mazoezi, maazimio yetu yalikuwa wazi. Tulikuwa na kiu ya kufanya mabadiliko makubwa muhimu kikosini, kufikisha ushindani katika kiwango cha juu zaidi na kuchangia uthabiti wa kikosi,” akasema Nuno.

Chini ya Nuno, Wolves walijizolea jumla ya alama 99 katika safari yao ya kujitwalia taji la Championship mnamo 2017-18 na wakakamilisha kampeni za kipute hicho kwa alama tisa zaidi kuliko Cardiff walioambulia nafasi ya pili. Kikosi hicho cha Wolves kilisajili ushindi mara 30 kutokana na mechi 46.

Katika msimu wao wa kwanza katika EPL mnamo 2018-19, Wolves walifuzu kwa hatua ya makundi ya Europa League na hivyo kurejea kunogesha soka ya bara Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.

Licha ya kuanza mapema kampeni zao za msimu wa 2019-20 ambapo walicheza jumla ya michuano 59 katika mashindano yote, Wolves waliambulia tena katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa jedwali la EPL na kutinga robo-fainali za Europa League.

Chini ya Nuno na msukumo wa wakala Jorge Mendes, Wolves walifaulu pia kusajili idadi kubwa ya wanasoka matata raia wa Ureno wakiwemo Joao Moutinho, Diogo Jota, Ruben Neves na Fabio Silva.

“Tumeshuhudia vipindi spesheli chini ya kocha Nuno. Hayo ni baadhi ya mambo ambayo hatuwezi kabisa kusahau kwa sababu yadumu kwa muda katika historia yetu. Hata hivyo, kila kitabu huwa na ukurasa wake wa mwisho,” akasema mwenyekiti wa Wolves, Jeff Shi.

Katika kipindi cha miaka 60 iliyopita, Wolves wamewahi kukamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara wa 12-bora mara saba pekee. Miwili kati ya misimu hiyo imekuwa 2018-19 na 2019-20.

Wolves kwa sasa wamepoteza wasimamizi watatu wakuu chini ya kipindi cha miaka miwili iliyopita walipotinga robo-fainali za Europa League. Hii ni baada ya kubanduka kwa Laurie Dalrymple aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji na Mkurugenzi wa Michezo, Kevin Thelwell.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

[ad_2]

Source link