Home » Kocha Carlo Ancelotti aondoka Everton na kutua kambini mwa Real Madrid – Taifa Leo
News

Kocha Carlo Ancelotti aondoka Everton na kutua kambini mwa Real Madrid – Taifa Leo

[ad_1]

Na MASHIRIKA

KOCHA Carlo Ancelotti, 61, ameondoka kambini mwa Everton na kurejea Uhispania kudhibiti mikoba ya Real Madrid kwa mara ya pili.

Mkufunzi huyo raia wa Italia aliwahi kuwanoa Real kwa kipindi cha miaka miwili kati ya 2013 na 2015. Anaagana rasmi na Everton baada ya kuhudumu uwanjani Goodison Park kwa kipindi cha miezi 18 pekee.

Ancelotti anamrithi kocha Zinedine Zidane aliyejiuzulu kambini mwa Real baada ya miamba hao wa soka ya Uhispania kukamilisha kampeni za msimu wa 2020-21 bila taji lolote.

Kuondoka kwa Ancelotti ugani Goodison Park kunasaza Everton katika ulazima wa kutafuta kocha wa sita chini ya kipindi cha miaka mitano.

Ancelotti ametia saini mkataba wa miaka mitatu kambini mwa Real walioambulia nafasi ya pili nyuma ya mabingwa Atletico Madrid kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) muhula huu.

“Nina heshima kubwa kwa kila mmoja anayejihusisha na Everton. Ni matarajio yangu kwamba watafanikiwa kutimiza maazimio mengi yaliyopo mbele yao,” akatanguliza.

“Japo nimekuwa nikijivunia muda wangu kambini mwa Everton, nilichochewa kubanduka baada ya fursa nzuri ambayo sikuwa nimetarajia kujitokeza. Nahisi kwamba maamuzi yangu ya busara ni bora hata kwa familia yangu wakati huu,” akasema Ancelotti.

Huku Real wakitarajiwa kumtambulisha Ancelotti kwa mashabiki wao mnamo Juni 2, 2021, Everton kwa upande wao wamesisitiza kwamba wana mpango wa “kuanza mchakato wa kumsaka mkufunzi mpya mara moja”.

Ancelotti anajivunia ufanisi wa kutwaa mataji 15 ya haiba katika taaluma yake ya ukufunzi na ni miongoni mwa wakufunzi watatu baada ya Bob Paisley na Zidane kuwahi kunyanyua mataji matatu ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Paisley alipata ufanisi huo akidhibiti mikoba ya Liverpool.

Ancelotti amewahi pia kunyanyua mataji ya Ligi Kuu akidhibiti mikoba ya AC Milan (Serie A), Chelsea (EPL), Paris St-Germain (Ligue 1) na Bayern Munich (Bundesliga).

Baada ya kuongoza AC Milan kunyanyua mataji mawili ya UEFA, Ancelotti aliwashindia Real taji hilo kwa mara ya 10 kwenye kipute hicho mnamo 2014 kabla ya kubanduka ugani Santiago Bernabeu mwaka mmoja baadaye. Real walitia kapuni mataji matatu ya UEFA wakinolewa na Zidane kati ya 2016 na 2018.

MAKOCHA WA EVERTON CHINI YA MIAKA 5 ILIYOPITA:

Kocha Tarehe ya kuondoka

Carlo Ancelotti Juni 2020

Marco Silva Disemba 2019

Sam Allardyce Mei 2018

Ronald Koeman Oktoba 2017

Roberto Martinez Mei 2016

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

[ad_2]
Source link